Jumatatu, 10 Julai 2017

HISTORIA YA MWANAMALUNDI

HEBU LEO MJUE VIZURI HUYU MTU WA MIUJIZA AITWAE NG'WANAMALUNDI SHUJAA WA WAKISUKUMA ALIYEWATESA WAJERUMANI.

Kwa wale waliopata kusoma historia au kusikia hadithi za makabila, hasa ya Wasukuma na Wanyamwezi, hawakukosa kusikia habari ya Ng’wanamalundi.
Mtu huyo aliyewahi kuutingisha utawala wa Wajerumani, alizaliwa katika ukoo wa kawaida akiwa mcheza ngoma mashuhuri, mwaka wa kuzaliwa kwake haufahamiki ila alifariki dunia mwaka 1936, akiwa tayari mtu mzima.

Watu wengi wamekuwa wakimjadili kwa maoni tofauti, wengine wakimsifu kama shujaa huku wengine wakihusisha uwezo wake na nguvu za giza.
Katika makala hii usahihi wa historia yake unaelezwa na mjukuu wake wa pili, Kishosha Sitta (80) mkazi wa Kijiji cha Mwalugulu wilayani Kahama mkoani Shinyanga, anayesimulia alivyomfahamu babu yake huyo.

Sitta anaanza kueleza kuwa jina halisi la babu yake halikuwa Ng’wanamalundi bali lilikuwa Igulu Bugomola, ambaye alizaliwa katika Kijiji cha Mwakubunga Nera wilayani Kwimba mkoani Mwanza.

Ng’wanamalundi alikuwa mtoto pekee wa kiume na wa mwisho kati ya wanne, kwa baba yake Bugomola na mama yake, Ngolo Igulu.
Sitta anasema Igulu (Ng’wanamalundi), alikuwa na tabia ya uzururaji tangu utotoni na mara nyingi haikuwa rahisi kumkuta nyumbani. Alikuwa mashuhuri kutokana na umahiri wake wa kucheza ngoma na mara nyingi alipokuwa akitembea mitaani alifuatwa na kundi kubwa la watoto.

“Hali hiyo iliwachukiza wazazi wengi wenye watoto waliokuwa wakiambatana naye, kiasi cha kumchukia hata Ng’wanamalundi mwenyewe, kutokana na watoto wengi hasa waliokuwa wakitoka familia za wafugaji kutoweka na hiki kilikuwa chanzo cha mifugo mingi kupotea baada ya kutelekezwa na watoto hao,” anasema Sitta.

Hali ya kuchukiwa kwa Ng’wanamalundi ilienea pale kijijini kiasi cha kuanza kumkebehi, hasa kutokana na umbo lake refu na miguu yake myembamba kuanzia magotini hadi kwenye makanyagio, ikiwa mirefu kuliko kawaida.
Sitta anasema hali hiyo ilisababisha kumdhihaki na kumwongezea chuki zaidi kwa wanakijiji wa eneo hilo waliodiriki kumtukana kwa lugha ya Kisukuma; “Mamirundi galyo lilihumbura bana bise” ikiwa na maana ‘mamiguu yake marefu linarubuni watoto wetu”.

Hapo ndipo ukawa mwanzo wa kufutika kwa jina la Igulu na kuwa Ng’wanamalundi, jina ambalo lilitokana na urefu wa miguu yake na kila kona walimuita hivyo.
Kadiri siku zilivyosonga mbele Ng’wanamalundi alizidi kujiimarisha katika kikundi chake cha ngoma ambayo ilivuta vijana wengi, pia baadaye ilitumika kama jeshi la kukodiwa na Watemi inapotokea vita.

Pamoja na wazazi kumchukia sana, lakini vijana walimpenda na kikundi chake kikubwa cha ngoma kilipendwa na kutumika katika sherehe mbalimbali kwenye familia za Kitemi za wakati huo.

Mwanzo wa miujiza
Sitta anasema Ng’wanamalundi na wenzake wawili walikwenda kwa bibi kizee mmoja kutafuta dawa itakayowasaidia katika shughuli zao za kucheza ngoma, ambapo bibi kizee huyo alikubali kuwasaidia.

“Tujagi lolo ngh’wiporu bana bane akiwa na maana kwamba twendeni sasa porini watoto wangu. Mwanamalundi aliongozana na wenzake pamoja na kizee huyo mpaka porini.

“Walipofika porini bibi Kizee huyo alikamata vinyonga watatu na kuwaekea vichwani, kwa kila mmoja na kuendelea kusonga mbele porini, baada ya kufika katikati ya pori nene, kizee aliwaambia wote wasimame,” anasimulia Sitta.
Anasema baada ya kusimama aliamuru kila mmoja achimbe shimo lenye urefu hadi kiunoni, na baada ya kukamilika kwa mashimo hayo aliwaambia wakusanye kuni na kuzitumbukiza.

Baada ya kazi hiyo kukamilika Sitta anasema walipekecha moto na kuziwasha zile kuni na moto uliposhika kasi aliwachukua wale vinyonga watatu na kuwawekea dawa mdomoni na kisha aliwatupia ndani ya moto huo, wakateketea wote.

“Ng’wanamalundi na wenzake wakiwa bado wanashangaa vinyonga hao kuungua, ghafla alitokea kifaru kwenye moto huo na kuanza kuwakimbiza hovyo na wote wakasambaritika na bibi kizee wao,” anasema na kuongeza;
Ngw’anamalundi alikimbia akapanda juu ya mti, kifaru alifika kwenye shina la mti na kuanza kuliparua kwa hasira na baadaye aliondoka kabla hajafika mbali alimuona yule bibi kizee akikutana na faru huyo.”

Anasema Ng’wanamalundi alishuhudia kifaru akimrarua rarua bibi kizee mpaka akafa, kisha kifaru alitoweka kusikojulikana huku akimuacha Ng’wanamalundi asijue la kufanya juu ya mti.

Sitta anasema: “Ng’wanamalundi baada ya muda alishuka juu ya mti na kwenda kwenye maiti ya yule bibi kizee, akaamua aibebe mgongoni airejeshe nyumbani, lakini kabla hajafika mbali alisikia sauti ikisema, “Igulu bajahe abiyo akiwa na maana Igulu wenzako wamekwenda wapi”.

Sauti hiyo ilimshtua Ng’wanamalundi ambaye alimshusha bibi kizee mgongoni mwake na akashangaa kumuona akiwa hai asiyekuwa na jeraha lolote, kama alivyokuwa baada ya kushambuliwa na faru.

“Igulu tujage ahante ugo waliwalinaga, akiwa na maana Igulu twende kwenye mti uliokuwa umepanda, Ng’wanamalundi aliongozana na bibi kizee huyo mpaka kwenye ule mti aliyachukua magamba ya mti yaliyokuwa yameparuliwa na faru,” anasema Sitta.

Baada ya zoezi hilo kukamilika bibi kizee huyo alimtengenezea dawa aliyokuwa akihitaji, na kisha Mwanamalundi alirejea kwao kuendelea na shughuli zake za ngoma aina ya Kahena, ambayo mpaka leo inaendelea kwa jina lingine la Wigashe.

Anakutana na Mtemi Chlya
Sitta anaongeza kuwa, Ng’wanamalundi akiwa katika harakati zake za kujiimarisha katika masuala ya dawa zake za ngoma, alienda kuchimba kwenye pori la Mwandutu huko wilayani Maswa sasa ni Wilaya ya Kishapu, ambalo lilikuwa katika miliki ya Mtemi Chalya.

Imeelezwa kuwa baada ya kufika katika pori hilo akiwa na wafuasi wake wakiendelea kuchimba dawa, ghafla alitokea Mtemi Chalya na kumuuliza; “Ubebe nani wakuwilaga kwiza ngh’wiporu lyane” akiwa na maana; “Wewe nani amekuambia kuja kwenye pori langu?”

Mwanamalundi alimjibu; “ Ubebe ulintemi wa banhu pye nu nene nding’wenekele wa maporu pyee.” Akiwa na maana “Wewe ni Mtemi wa watu wote na mimi ni mmiliki wa mapori yote”. Kauli hiyo ilimuudhi Mtemi Chalya.
Anasema, kufuatia kauli hiyo Mtemi Chalya aliita jeshi lake kwa lengo la kuja kumkamata, lakini walishangaa baada ya kufika katika eneo waliloelezwa na Mtemi wao kuwa Ng’wanamalundi anatakiwa kukamatwa na kuuawa, lakini walishindwa baada ya kukuta simba wengi sana.

Jeshi hilo na Mtemi ilibidi kukimbia kujiokoa kwani simba hao walianza kuwashambulia, wengine walitawanyika ovyo na baadhi yao wachache tu ndiyo walionusurika.

Lakini cha kushangaza walipofika walimkuta Ng’wanamalundi na wafuasi wake wakimalizia kula chakula nyumbani kwa Mtemi Chalya, ambaye hata yeye alichanganyikiwa na kushindwa kuongea lolote.

Sitta anasema, Ng’wanamalundi baada ya kumaliza kula chakula kwa Mtemi Chalya aliondoka na wafuasi wake na akapitia kwenye lile pori akachimba dawa zake na kuondoka kwenda kuendelea na maisha yake.

“Katika ngoma zake; Ng’wanamalundi alikuwa na tabia ya kuwatahadharisha mashabiki wake kuacha kwenda wakiwa wamejipaka dawa yoyote ile, anasema. Aliwaambia: “Bing’we akwiziza munho wibilaga bugota bosebose ulu kutora akotora henaha,ulo nsabo akupandika heneha.”

Kauli hiyo ilikuwa na maana nyie asije mtu amejipaka dawa yoyote hapa kama ni kuoa, ataoa hapahapa kama ni mali atapata hapahapa, hata hivyo kuna wale walipuuza kauli hiyo kwa kuja wamejipaka dawa kwa lengo la kujipima uwezo wa dawa zao. Lakini hawakufanikiwa na badala yake walikufa.

Akiwa anaendelea na ngoma yake wananchi wa Kijiji cha Sekke waliibiwa ng’ombe wengi sana na watu kutoka Kabila la Wamasai ambao walienda kuwahifadhi katika Pori la Mwanima karibu na Kijiji cha Bubiki. Ng’wanamalundi na kikosi chake waliondoka Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza na kuelekea Sekke wilayani Kishapu mkoani Shinyanga kwa lengo la kusaidia kuzikomboa ng’ombe zilizoibwa. Hata hivyo kabla hawajafika uwanja wa vita, Ng’wanamalundi alifanya utabiri wake uliotokana na nguvu ambazo alizipata kutoka kwa Bibi Kizee wa porini. Sitta anasema aliwaambia kuwa kabla ya vita, itatokea mvua kubwa sana na ikikatika watakuja ndege hai aina ya mwewe watakaokuwa wanazungukazunguka kwenye zile ng’ombe na hapo sasa wafuasi wake wakate miti mifupi mifupi (Lubugu).

Sitta anasema utabiri huo ulitimia, kwani mvua ilinyesha kubwa sana na baada ya kukatika wale mwewe walijitokeza wengi sana wakawa wanazunguka kwenye zile ng’ombe na ndipo yale mapigano ya Wamasai na wafuasi wake yalipoanza. Aliwaeleza kuwa baada ya kuwa na fimbo ya Lubugu wale wenye upinde na mishale watakaa nyuma na kazi yao watakuwa wanazipiga zile ngao za Kimasai na zikidondoka chini ndipo wenye pinde na mishale waanze kushambulia. Mwanamalundi alipigana hiyo vita ya Wamasai mpaka akazirejesha zile ng’ombe na aliwatokomeza Wamasai mpaka kwenye mpaka wa Mto Manonga unaotenganisha Tinde Shinyanga na Nzega mkoani Tabora. Hapo ndipo ilibainika Wamasai hao walikuwa wametumwa kuiba ng’ombe Usukumani na Mtemi Tinginya wa Busongo Nzega, ambapo baada ya vita hiyo Ng’wanamalundi na kundi lake walirudi Sekke na kupewa jina la Kishosha Mang’ombe tafsiri ikiwa ni mrudisha ng’ombe. Baada ya vita hiyo Ng’wanamalundi alirudi nyumbani kwao wilayani Kwimba kuoa, lakini bahati mbaya ilimkuta, kwani kila mke aliyejifungua, mtoto alikufa.

Baba yake Bugomola akaenda Ntuzu kwa sasa Bariadi kufanyiwa tambiko kuhusu uzazi kwa mwanaye. Akiwa huko Ntuzu, Bugomola alielezwa mwanaye Ng’wanamalundi hatapata mtoto kwa wake zake alionao. Hivyo aoe msichana atakayempata upande wa Mashariki ambaye atakuwa akiitwa Nkamba na atazaa watoto watatu; wa kwanza ataitwa Sitta, wa pili Ngassa na wa tatu Marieta. Baada ya kurudi Bugomola, haikumchukua muda mwanaye Ng’wanamalundi akapata msichana akaoa na akaendelea na shughuli yake ya kuendesha kikundi cha ngoma. Ng’wanamalundi kuwekwa kizuizini Akiwa anaendelea na ngoma zake katika maeneo ya Kanda ya Ziwa, Sitta anasema siku moja yeye na kikundi chake walipokuwa wakiburudisha katika maeneo ya Bukumbi mkoani Mwanza, wafuasi wake walipumzika kwenye mti mkubwa ambapo pia kilikuwa Kituo cha Wajerumani, Ng’wanamalundi aliwaambia wafuasi wake waondoke waende kwenye ngoma, wafuasi wake waligoma wakadai wanapumzika kwenye kivuli hicho ili wavute sigara. Baada ya kuwabembeleza vya kutosha akabaini hawataki kumsikiliza ndipo alipounyooshea kidole ule mti akisema “Ngh’walemelaga hanti gunugo aliyo gumaga,” akiwa na maana “Mmekatalia kwenye mti huo huku ukiwa umekauka.” Ghafla mti huo wote ulikauka.

Kuona hivyo wafuasi wake wakaondoka wote kwenye huo mti wakaenda kuendelea na ngoma yao ambayo walicheza katika eneo la Bukumbi na Busagara karibu na Mji wa Mwanza na walipomaliza walirejea Kwimba. Akiwa Kwimba alicheza ngoma moja na Gindu Nkima, ngoma hiyo ilikuwa ngumu kwake ilichezwa sehemu za Mwanagwa. Baada ya kuwa amezidiwa Ng’wanamalundi, wapishi wake walimfuata na kumtaka awasaidie namna ya kupata kuni za kupikia. Kutokana na uharaka aliokuwa nao Ng’wanamalundi alielekeza kidole chake kwenye miti ya minyaa iliyokuwa mbele yake huku akisema “Batemagi pye abenababa mkazugile,” akiwa na maana “Yakateni yote haya mkapikie.” Baada ya kauli hiyo minyaa yote ilikauka na kuwa kuni na wafuasi wake walikata wakaenda kupikia chakula. Akiwa katika ngoma hiyo wakati huo barabara ya kutoka Shinyanga kwenda Mwanza ilikuwa inachongwa na manamba waliokuwa wakikamatwa na Wajerumani kwa ajili ya kazi hiyo, Gavana wa Kijerumani wa eneo la Mwanza alipita eneo hilo akiwa amepanda punda alikuta kazi imesimama, alipohoji kwanini kazi imesima

alielezwa wananchi wote wamekwenda kwenye ngoma ya Ng’wanamalundi. Kitendo hicho kilimchukiza sana Mjerumani huyo, ambaye aliondoka akaenda Mwanza na baada ya siku mbili walikuja askari waliomkamata Ng’wanamalundi na kumfunga mnyororo na watuhumiwa wengine walipelekwa Mwanza na kuwekwa gerezani.

Kosa hilo kwa utawala wa Ujerumani lilihesabiwa kuwa ni uhaini wa kupinga utawala wao hivyo alitakiwa kupewa adhabu ya kunyongwa. Kabla hajapelekwa Mwanza, kwa kuwa ilikuwa ni safari ya kwenda kunyogwa, alipelekwa nyumbani kwa wazazi wake kuaga. Alipofika nyumbani kwao alimpa mama yake shoka aliloliweka pembezoni mwa ukuta chumbani na maziwa, huku akitoa maelekezo. “Mayu imbasa yeneye ulu yulina ng’wigulya mumhonatwalwa ulu yika hase mumhonashoka amabele genaya ulu guganda mumhonacha, ulu gita lububhi mumhonasata.” Akiwa na maana hii shoka ikipanda juu basi nitakuwa nimepelekwa ikishuka chini nitakuwa nimerudishwa.” Sitta anasema Ng’wanamalundi aliendelea kumpa maelekezo mama yake kuwa haya maziwa yakiganda atakuwa amekufa na pindi yakipata utando atakuwa anaumwa, baada ya maelezo hayo Ng’wanamalundi alipelekwa Mwanza gerezani ambako alikutana na Mtemi Makongoro wa Mwanza. Siku iliyofuata walitolewa wote ambapo Sitta alieleza kuwa walikutana pia na mganga aliyemtabiria kuzaa watoto watatu ambaye naye alikuwa amekamatwa kwa kosa la kupiga ramli iliyosababisha mauaji ya kishirikina.

Asubuhi kila mmoja alisomewa mashtaka yake ambapo Ng’wanamalundi alisomewa mashtaka matatu, shtaka la kwanza kuukausha mti uliokuwa ukitumiwa na maofisa wa utawala wa Wajerumani kama kituo cha kupumzikia huko Bukumbi Mwanza. Shtaka la pili kuwatungia na kuwaimbia nyimbo mbaya Wajerumani na la tatu ni kukwamisha ujenzi wa Barabara ya Mwanza kwenda Shinyanga. Ng’wanamalundi alidaiwa kuchezesha ngoma eneo la Mwanangwa hali iliyosababisha wafanyakazi wa manamba waliokuwa wakilima barabara hiyo kuacha na kwenda kuangalia ngoma yake hali iliyowachukiza Wajerumani…

Ijumaa, 7 Julai 2017

SHAIRI LA SIBANDUKI

SIBANDUKI

Kama kidole na Pete,
Au ulimi na mate,
Milele takuwa wote,
SIBANDUKI.

Mapigo yenda ta ta ta,
Mie kwako ni zezeta
Wala siwezi kujuta,
SIBANDUKI.

Mtasema msemavyo,
Kuchongea mjuavyo,
Nitabaki hivyo hivyo,
SIBANDUKI.

Tumependana wenyewe,
Tunapeana wenyewe,
Tunafurahi wenyewe,
SIBANDUKI.

Waongee Siku kucha,
Penzilo halitochacha,
Daima sitakuacha,
SIBANDUKI.

Waseme maneno yote,
Ya duniani kote,
Hadi wakauke mate,
SIBANDUKI.

Kiangazi na masika,
Siku mwezi na miaka,
Kwa kimbunga na ghalika
SIBANDUKI.

Hata nichomwe mikuki,
Au risasi lukuki,
Kwako mwandani sing'oki,
SIBANDUKI.

Mahakama za kitaifa,
Au za kimataifa,
Waninyonge hadi kufa,
SIBANDUKI.

Jumatatu, 8 Februari 2016

Uhusiano wa Sintaksia na Matawi mengine ya Isimu



Dhana ya sintaksia imejadiliwa na wanazuoni mbalimbali ;
            Massamba na wenzake (1999:34) anasema “sintaksia ni utanzu wa sarufi unaojihusisha na uchunguzi wa mpangilio wa maneno katika sentensi na uhusiano wa vipasho vyake”. Wanaendelea kusema, utanzu huu huchunguza sheria  au kanuni zinazofuatwa katika kuyapanga maneno ili yalete maana inayokubalika na kueleweka katika lugha husika.
           Habwe na Karanja (2004) wanasema “sintaksia ni utanzu wa isimu unaoshughulikia muundo wa sentensi na elementi nyingine zinazounda sentensi kama vile kategoria za maneno, vikundi na vishazi”
        TUKI (2004)anasema “sintaksia ni tawi la isimu linaloshughulikia uchanganuzi wa taratibu na kanuni za mahusiano baina ya maneno katika tungo” kwa ufupi sintaksia ni tawi la isimu ambalo linachunguza muundo wa tungo pamoja na uhusiano wa vipashio hivyo vinavyounda tungo ambayo ni nukta pacha, neno, kirai na kishazi.
           Kwa ujumla sintaksia ni tawi la isimu ambalo linahusu namna maneno yanavyoungana na kuhusiana kirai, kishazi na sentensi. Sintaksia inachunguza namna maneno yanavyojipanga katika sentensi kwa kuzingatia kanuni za sarufi ya lugha husika.
         Kwa hiyo kutokana na kwamba sintaksia pia ni kitengo mojawapo kinachounda maarifa ya lugha, kwamba, sintaksia haiwezi kutenganishwa na vitengo vingine vya lugha kutokana na uhusiano mkubwa uliopo baina ya vitengo hivi. Vitengo hivi hutegemena na kuathiriana. Hivyo basi tunaweza kuonesha jinsi sintaksia isivyoweza kutenganishwa na vitengo vingine vya lugha yaani fonolojia, mofolojia na semantiki kama ifuatavyo:
Uhusisno uliopo kati ya sintaksia na fonolojia.
          Massamba na wenzake (1999:34) wanasema “fonolojia ni uchambuzi wa mfumo wa sauti katika lugha mahususi” Ni jinsi ambavyo vitamkwa au sauti za lugha zinavyoungana ili kujenga maneno yanayokubalika katika lugha. Ni dhahiri kwamba kuna uhusiano usio na mashaka kati ya sintaksia na fonolojia kwa sababu hatuwezi kuwa na miuundo mikubwa bila kuwa na mpangilio sahihi wa sauti katika lugha.
Mfano 1. ‘anacheza’ hili ni neno lakini pia ni sentensi, hivyo linaweza kuchanganuliwa            kifonolojia kama, /a/n/a/ch/e/z/a/. kwa hiyo mpangilio sahihi wa sauti hizo ndizo zinazounda neno ‘anacheza’.
Mfano 2 (a). neno “debe” neno hili limeundwa na konsonanti irabu konsonanti irabu (KIKI).
           2. (b). “edbe” hili limeundwa na irabu konsonanti konsonanti irabu (IKKI).
Katika mfano 2a, neno “debe” lina maana na limefuata kanuni na mpangilio unaokubalika katika lugha ya Kiswahili, lakini katika mfano 2b neno “edbe” halina maana katika lugha ya Kiswahili kwa sababu halina mpangilio sahihi wa vitamkwa au fonimu.
Kwa hiyo mpangilio sahihi wa sauti katika maneno ndio husaidia kupata vipashio vikubwa zaidi katika lugha kama vile kirai, kishazi na sentnsi. Kwa hiyo sintaksia na fonolojia haviwezi kuenganishwa.
Uhusiano uliopo kati ya sintaksia na semantiki.
        Habwe na Karanja wakimnukuu Richard na Wenzake (1985) wanasema “Semantiki ni stadi ya maana. Semantiki ni utanzu unaochunguza maana katika lugha ya mwandamu”. Wanaendelea kusema semantiki hutafiti maana za fonimu, mofimu, maneno na tungo. Hivyo kutokana na fasili hii maana hushughulikiwa katika vitengo au viwango vyote vya lugha ambavyo ni fonolojia, mofolojia na sintaksia. Kwa mfano,
1               Mtoto mtiifu amefaulu mtihani.
2                Mtihani mtoto amefaulu mtiifu.
3              Mtiifu mtoto mtihani amefaulu.
Katika mifano hii sentensi (1) ina maana kutokana na kwamba imefuata mpangilio sahihi wa maneno katika tungo na sentesi zilizobaki hazina maana kutokana na sababu kwamba hazijafuata mpangilio ulio sahihi wa kimuundo katika lugha ya Kiswahili. Kwa mantiki hii, kwa kuwa semantiki hushughulikia viwango vyote vya lugha, basi hushughulikia pia kiwango cha sintaksia ambapo huangalia maana za tungo, kwani tungo lazima ikubalike kwa wazungumzaji wa lugha husika, pia tungo lazima ilete maana. Kwa mantiki hiyo kuna uhusiano usio na mashaka kati ya sintaksia na semantiki kwa sababu mpangilio sahihi wa maneno katika sentensi ndiyo huleta maana na bila mpangilio sahihi wa maneno maana hupotea.
Uhusiano uliopo kati sintaksia na mofolojia.
        Besha (2007:49) anasema “mofolojia ni taaluma inayojishughulisha na kuchambua muundo wa maneno katika lugha’.Pia Rubanza (1996:1) anasema “mofolojia ni taaluma inayoshughulikia vipashio vya lugha katika kuunda maneno”. Maumbo ya kimofolojia huathiri vipengele vingine vya kisintaksia kama vile kipengele cha umoja na wingi, katika maumbo ya kimofolojia ndicho kinachoathiri umbo linalofuata jina na kuathiri muundo wa sentensi nzima. Kwa mfano,
1                        Mtoto alikuwa anajifunza kusoma.
2                        Watoto walikuwa wanajifunza kusoma.
Katika mifano hii kiambishi m- na wa- katika upande wa kiima vimeathiri utokeaji wa viambishi a- na wa- katika upande wa kiarifu. Hivyo taaluma ya sintaksia na mofolojia haziwezi kutenganishwa.
            Kwa ujumla sintaksia kama tawi mojawapo la isimu linauhusiano wa moja kwa moja na matawi mengine kwani haiwezi kutenganishwa na vitengo vingine vya lugha kutokana na uhusiano mkubwa uliopo baina ya vitengo hivi. Hutegemeana na kuathiriana kwa kiasi kikubwa, mfano huwezi kupata mofolojia bila kupitia ngazi ya fonolojia na pai huwezi kuwa na ngazi ya sintaksia bila kupitia ngazi ya fonolojia na mofolojia lakini vitengo vyote hivi hutawaliwa na kitengo cha semantiki ili kuleta mawasiliano miongoni mwa wazungumzaji.






                                          MAREJEO
Besha, R.M. (2007). Utangulizi wa Lugha na Isimu. Dar es Salaam: Mackmillan Aidan
Habwe, J na P. Karanja (2004). Misingi ya Sarufi ya Kiswahili. Nairobi: Phoenix Publishers Ltd.
Massamba, D.P.B na wenzake (1999). Sarufi Miundo ya Kiswahili Sanifu: Sekondari na Vyuo.          Dar essalaam: TUKI.
Rubanza, Y.I (1996). Mofolojia ya Kiswahili. Dar es salaam: Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.
TUKI (2004). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Dar es salaam: TUKI.

Dhana ya Nadharia



Dhana ya nadharia imejadiliwa na wanazuoni mbalimbali ambao wamekuja na mitazomo tofauti tofauti kama ifuatavyo;
           Kwa mujibu wa Wamitila, (2003:22) “nadharia ni mawazo, dhana au maelezo yanayotolewa kuelezea hali fulani : chanzo chake, muundo wake, utenda kazi wake na mwingiliano wake wa ndani na nje”
          TUKI (2004:300) wanasema “nadharia ni mawazo, maelezo au mwongozo uliopangwa ili kusaidia kueleza, kutatua au kutekeleza jambo fulani”
Fasili hii ya TUKI inafanana kwa kiasi fulani na fasili ya Mdee (2011) anayefasili nadharia kuwa ni mpango wa maneno uliotungwa ili kuelekeza jinsi ya kufanya au kutekeleza  jambo fulani. http://kapeleh.blogspot.com/2014/05/nadharia-za-maana.html
Kwa msingi huo nadharia hubeba mawazo ,dhana au maelezo yatolewayo kwa nia au lengo la kueleza hali fulani, chanzo,muundo, utendaji na mwingiliano wa ndani na nje.
Kuna nadharia mbalimbali ambazo zimejadiliwa na wanazuoni mbalimbali, baadhi ya nadharia hizo ni pamoja na nadharia ya maana, nadharia za kifalsafa, kihistoria, nadharia ya fasihi, nadharia za chimbuko la lugha ya Kiswahili, nadharia ya chimbuko na chanzo cha lugha.
             Naye Wafula  na Njogu (2007:7) wamefasili dhana ya nadharia kama ni jumla ya maelekezo yanayomsaidia msomaji au mhakiki kuifahamu kazi ya fasihi kwa kufuata utaratibu maalumu. Fasili hii imeegemea hasa katika nadharia ya uhakiki wa fasihi. Pia imetaja vitu muhimu kama vile, maelekezo ambayo ndiyo yanamuongoza msomaji au mhakiki ili asivuke mipaka ya mawazo ya hiyo nadharia aitumiayo ili kufanikisha kazi kwa ufasaha.
               Pia Sengo (2009:1) anafasili nadharia kuwa ni wazo kuu fikra kuu, mwongozo mkuu wa mtu, watu au jamii ya pahala fulani, wakati fulani na kwa sababu fulani. Kwa mantiki hiyo nadharia ni dira au mwongozo wa kulikabili jambo kifalsafa, kidini, kimantiki, kijamii na kiutamaduni.
             Ili kuweza kudhibitisha maelezo yaliyotolewa na wataalamu mbalimbali kuhusu dhana ya nadharia ni vyema kuangalia mfano mmojawapo wa nadharia, ambayo ni nadharia ya sarufi. Katika nadharia hii kuna wanaisimu mbalimbali wamejitokeza kuelezea nadharia ya sarufi kwa mitazamo tofauti tofauti ambayo imeweza kuibua nadharia mbalimbali za sarufi kama vile nadharia ya sarufi mapokeo, nadharia ya sarufi msonge na nadharia ya miundo virai.
                Katika nadharia ya sarufi mapokeo Mgullu (1999:68) anasema ni sarufi ya kale iliyochambuliwa kwa kutumia vigezo vya lugha za Kilatini na Kigiriki zilizokuwa na mnasaba mmoja, yaani zilikuwa na asili moja. Kwa mantiki hiyo lugha za Kilatini na Kigiriki zilikuwa kama kiolezi cha kuchanganulia lugha nyingine ikiwemo lugha ya Kiswahili. Kwa mfano wanaisimu wa Kilatini waliposema kuna aina nane za maneno na baadhi yao katika lugha ya Kiswahili wakasema kuna aina nane za maneno bila kuzingatia kwamba lugha hutofautiana. Pia nadharia hii ilijikita na sentensi sahili, haikujishughulisha na miundo  kwa marefu na mapana.
              Baada ya kuonekana sarufi mapokeo ina udhaifu mkubwa iliibuka nadharia ya sarufi msonge. Mgullu (1999:70) anaiona sarufi hii ni sehemu ya mkabala wa kimapokeo isipokuwa mkabala huu unaiona lugha kuwa ni mfumo mkuu yenye mifumo mingi ndani yake kama vile mifumo midogo ya fonolojia, mofolojia, sintaksia na semantiki.
             Katika karne ya kumi na nane na kumi na tisa sarufi mapokeo ikafikia kilele ndipo ikaibuka nadharia ya sarufi miundo virai. Nadharia hii inadokeza kuwa tungo imeundwa na viambajengo ambavyo vina uhusiano na vipo kidarajia. Kwa mujibu wa Mgullu (1999:70) isimu muundo imejitokeza sana katika maandishi ya akina Harris, Ferdinand De Saussure, Trubetzkoy na Bloomfield.
Katika mkabala huu lugha ilionekana kuwa na viambajengo kama vile: maneno, kirai, kishazi na sentensi na kwamba viambajengo hivyo vina uhusiano mkubwa na viko katika kidarajia toka chini hadi juu. Kwa mfano
        Mkulima bora analima vizuri
Katika sentensi hii kuna uhusiano wa karibu wa viambajengo vifuatavyo; N+V yaani nomino “mkulima” na kivumishi “bora”, hali kadhalika, T+E, yaani kitenzi “analima” na kielezi “vizuri”.
Katika mkabala huu dhana ya uchamko ikaibuka kuonyesha uwezekano wa kuzalisha sentensi bila kufika kikomo. Kwa mfano,
       Waziri fisadi amekamatwa jana na rais akiiba fedha za wananchi.
Hivyo ili kuwa na nadharia inayokubalika katika jamii ni muhimu kuzingatia fasili ya Sengo, (2009:1) ambaye anasema kuwa “nadharia ni wazo kuu, fikra kuu, mwongozo mkuu wa mtu, watu au jamii ya pahala fulani, wakati fulani na kwa sababu fulani”.
Kwa mantiki hiyo nadharia ni dira au mwongozo wa kulikabili jambo kifalsafa, kidini, kimantiki, kijamii na kiutamaduni.
              Kwa ujumla nadharia huchukuliwa kuwa ni dira ya kumwongoza mtafiti au mchambuzi kulikabili na kulielezea vyema jambo fulani kwa mtazamo unaotazamiwa kuwa imara zaidi kuliko ule wa nadharia nyingine. Nadharia hutoa mwongozo katika utatuzi wa jambo fulani ambalo halijaweza kuhakikishwa ukweli wake. Ni mawazo , maelezo au mwongozo uliopangwa ili kusaidia kutatua au kutekeleza jambo fulani kifalsafa, kidini, kimantiki, kijamii na kiutamaduni.


             MAREJEO
http://nenothabiti.blogspot.com/p/fasihi.html by Anonymmous Said, 31 October 2013 at 9:39AM
Sengo, T.S.Y.M (2009) Fasihi za Kinchi. Dar es Salaam: The Trustees of Al Amin Education and Research Academy
TUKI (2004). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Dar es salaam: TUKI
Wamitila, K.W (2003) Kichocheo cha Fasihi Simulizi na Andishi. Nairobi: Kenya Focus   Publications Ltd
Wafula, R.M & Njogu, K (2007) Nadharia za Uhakiki wa Fasihi. Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation